FURAHA YANGU ILIPO SEASON 2 EPISODES 13 - 18

 


FURAHA YANGU ILIPO
SEASON TWO 13 HADI 15

Na Mr AB ENTMENT

KIPENGELE CHA 13
BAADA YA KUMI NA TANO (15)
Ilikuwa ni kama masihara lakini ni kweli na wazi kwamba baada ya Maulid kupata ajali Samawati hakuwahi kufika tena hospitalini, hakuwa na nia ya kweli ya kumsaidia licha ya kwamba yeye ndiye chanzo cha Maulid kupata tatizo la kupigwa na kuumizwa vibaya.

Maulid aliendelea kubaki hospitali, kila siku Tricia ndiye alikuwa akimuhudumia chakula na hata vitu vingine.

hata hivyo hii hali ilipelekea deni la hospitalini kufika hadi laki saba kwa kipindi chote alichokuwa pale, pamoja na matibabu, angalau alikuwa na uwezo wa kuilipa hiyo pesa hata kidogo.

Vile vile ugomvi mkubwa ulizuka kati ya Tricia pamoja na Frank, kila mara Frank alilalamika kwanini ukaribu wa Tricia na Maulid unazidi kuwa mkubwa wakati wao wameshaachana kitambo

“Hivi Frank unakasirika kila siku....”

“Sitaki umsaidie huyo Maulid....”

“Jamani” alisema binti

“Ndio hivyo...kwanza nikuambie kitu? Tangu ukutane naye hunisikilizi chochote nachokuambia”

“Nikusikilize nini? Hivi una roho ya aina gani, ina maana mtu akipata matatizo huwezi kumsaidia?”

“Kwa hiyo pale hospitalini huyo tu ndiye umeona ana matatizo? Mbona husaidii wengine?”

“Niache bwana....yule mi namjua toka mda”

“Poa endelea kumjua” alisema Frank kwa hasira huku akimuangalia binti anavyokunja nguo za Maulid alizokuwa amekuja kuzifua pale nyumbani

“Sawa” 
Tricia baada ya kumaliza hiyo shughuli, alianza kupakulia chakula kwenye kikontena, alihitaji kumpelekea lakini baada ya kupakua tu hivi, Frank alikishika kikontena na kukitupa nje chakula kikamwagika kule...akaona haitoshi akabeba na sufuria akatupa nje kikamwagikia kule

“Frank” binti alimuita kwa hasira huku akimnyooshea mwiko

“Mjinga nini? Yaani chakula upikie kwangu halafu umpelekee hawara wako” alisema mtaalamu yaani nusu tu binti ampige na mwiko lakini alisita maana alikuwa ana nidhamu ya hali ya juu.

Frank akaona udhaifu wa binti akaamua kuvuruga na zile nguo binti alizokuwa amezipanga vizuri... Tricia akajikuta ameumia mpaka ametokwa na machozi, yaani hasira zilikuwa ni nyingi sana.

Hakujali sana, alienda akaosha kikontena akaweka kwenye mfuko, akazikusanya zile nguo halafu akaondoka pale nyumbani.

Tricia alipita hotelini na kwenda kununua chakula halafu akampelekea Maulid hospitalini.

Maulid alikuwa na nafuu kabisa, licha ya kuchechemea alikuwa anaweza kuketi vizuri na hata kula peke yake.

Usoni alikuwa na makovu kibao binti akamtazama kwa hisia na kumuambia “Kuna dawa nitakuletea jioni ukipaka tu makovu yote yanaisha unakuwa kama zamani”

Maulid alimtazama Tricia usoni, bado alikuwa ni chaguo sahihi katika maisha yake, alijikuta anatokwa na machozi halafu akamuambia “Tricia asante kwa unavyonijali” alisema na kufuta machozi, binti akatoa kitambaa na kumfuta usoni

“Usijali...mi nipo kwa ajili yako” alisema

“Anyway...nimeruhusiwa kuondoka”

“Kweli?”

“Ndio...lakini sijui ninaenda wapi” alisema Maulid “Nilitamani niendelee kubaki hapa mpaka niwe mzima kabisa kama zamani ila, kila ninavyozidi kukaa basi deni linazidi”

“Imefika shilingi ngapi?”

“laki saba na elfu arobaini na tisa”

“Duuh....sasa itakuwaje?”

“Hamna namna Tricia...naamini unaona mateso nayopitia...naomba unisaidie niondoke hapa”

“Nakusaidiaje sasa? Mi sina hela eti Maulid ningekusaidia haki ya Mungu”

“Basi usijali”

“Maulid, usiumie sana sawa? Nakupenda” alisema binti

“Najua unanipenda....lakini upande mmoja najuta kuonana na wewe?” alisema na kufuta machozi “Na upande wa pili nashukuru kukutana na wewe katika maisha yangu”

“Kwanini unajuta kuonana na mimi Maulid?”

“Tricia” alisema mtaalam kwa majonzi “Mimi kama binadamu siku zote natamani niishi maisha marefu maana nimeumbiwa roho ya kuogopa kifo.....ndio maana nashukuru kuonana na wewe katika maisha yangu....maana umenifanya mpaka leo nipo hai”

“Kivipi Maulid?”

“Lakini kwa mateso ambayo nimepitia tangu nilipoonana na wewe, kiukweli bora nisingekuona, ungekuta leo hii mimi ni marehemu” aliongea huku akilia sana mtoto wa kiume ilikuwa kama vile ni msibani

“Maulid bwana....mi sikuelewi hata”

“Tricia nikuambie kitu kimoja.....?”

“Niambie”

“Siku ya kwanza ulipokuja kulala kwangu....nilikuwa najiandaa na safari kwenda na marafiki zangu njombe lakini, ulinifanya nikabaki kwa sababu nilikupa thamani kubwa kuliko kazi yangu”

“Nisamehe kwa hilo Maulid”

“Hukunikosea hata chembe...kwa sababu siku ile marafiki zangu walienda wakapata ajali na walifarik wote kwa pamoja”

“Wewe!!!” binti aliongea kwa mshtuko huku akimshangaa jamaaa

“Ndio....yaani kama usingekuja, basi ungekuta nami nimeshafariki muda mrefu sana”

“Maulid....usilie sasa...kwa hiyo walikufa??”

“Ndio....na ndio maana muda mwingine nakuona wewe umebeba nyota ya maisha yangu....bila wewe ungekuta nimeshasahaulika...nashukuru sana”

“Usijali kula sasa”
Zilikuwa ni story zenye kujenga hisia kali za maumivu kwa pande zote mbili, kila mmoja aliumizwa na story zile
ITAENDELEAA

KIPENGELE CHA 14
Tricia aliondoka hospitali mida ya saa kumi, alikuwa ameshaomba ruhusa ya kutokuhudhuria usiku ule. Alimpigia simu baba mdogo wake, aitwaye Isaac
“Ba mdogo shikamoo”

“Marahaba mtoto mbaya”

“Ubaya wangu nini tena jamani?”

“Yaani, kwa hiyo kuja kunisalimia mara moja ukaona ndiyo inatosha? Umenifanya natenda dhambi kila siku kumuambia baba yako uongo...anyway unaendeleaje?”

“Salama tu.....nataka sasa nihamie huko kwako maana nimechoka kuishi na rafiki yangu ananikorofisha sana” alisema

“Mmmh...kweli?”

“Ndio...nitapata nafasi?”

“Of course yes...njoo tu”

“Sawa ninataka nijiandae hapa nije leo jioni”

“Sawa usijali mwanangu”

“asante ba mdogo” binti alisema na kukata simu.

Tricia alienda nyumbani, akamkuta Frank amejifungia ndani akamgongea “Frank....Frank.....” lakini Frank akawa kimya “We Frank nifungulie” lakini Frank kimya

Tricia akasogea dirishani na kuligonga, ndipo Frank akapunguza sauti ya redio “Nini?” Frank aliongea kwa jeuri

“Naomba nifungulie”

“Ah unasumbua bhaana” alisema hasira kisha akafungua mlango.

Tricia aliingia ndani akaanza kuokota kila kilichokuwa cha kwake, anashindilia kwenye begi 

“Vipi mbona unapanga vitu?”

“Nimeamua niondoke”

“Unaenda wapi?”

“Ulidhani sina ndugu huku Mbeya?? Uliona ulichonifanyia asubuhi ni kitu kizuri sana ee? Halafu hata sasa hivi nakugongea mlango unakausha kama usikii si maana yake hutaki usumbufu? Basi baki na geto lako mi naenda kwa ndugu yangu”

“Mh yamekuwa hayo tena?”

“Niache” binti alisema na kuzidi kujiandaa mpaka akamaliza.

Baada ya kuamini kila kitu kimekaa sawa, binti aliondoka bila hata kumuaga, akatoka nje ya geti na kuita bajaji, impeleke Forest

Baada ya muda binti alifika kwa ba mdogo wake, alikuwa anapajua, japo alimkosa lakini alimkuta mkewe akiwa anapika chakula cha usiku. Waliongea mengi alimkaribisha sana sana sana...na alikuwa ameokoka mno

Usiku saa mbili, bado Maulid alizunguka katika ubongo wake, alikuwa anapata taabu sana kwa sababu ya mwanaume yule yaani hakujua kwanini amemtawala kiasi kile.

Mtoto wa kike alijikuta anapata shida, Maulid alikuwa hana simu, ilikuwa imepotea siku ile alipopigwa na Iddi.

Tricia aliweweseka, hakuweza kumpelekea chakula kwa sababu alikuwa mbali kidogo na pale alipokuwa hospitalini. Vile vile alikuwa kwa ba mdogo hivyo kutoka toka isingewezekana kirahisi ili kuweza kuonyesha nidhamu kwa ndugu.

Tricia hakuweza kuvumilia, alichukua simu akampigia nesi mmoja ambaye alikuwa zamu ya usiku ule, alikuwa anaitwa Flora Ngoma

“Madama Flora” alisema Tricia baada ya Flora kupokea simu

“Yes, how are you”

“I’m fine, how about you my dear?” alisema binti

“I am fine too”

“Samahani dada F, eti upo hospitalini?”

“Ndio...Nambie”

“Ninaomba kuongea na Maulid kuna kitu cha kumuambia”

“Sawa ngoja nimpelekee simu” Flora alisema

“Ok”

Tricia alikata simu, ndipo Flora alipoenda kule wadini kumtazama akakuta jamaa ameketi anawaza sana
“Maulid...hujalala?”

“Siwezi nikapata usingizi kwa mfano” alisema mauldi

“Sawa, Tricia anaomba kuongea na wewe kwenye simu”

“Sawa”

Flora alimtumia ujumbe binti Tricia ampigie naye alifanya hivyo kwa haraka, ikabidi Flora amuache aongee peke yake akiamini lazima kuna mambo binafsi wanataka waongee

“Maulid umeshindaje?” alisema Tricia

“Niko powa tu” alijibu Maulid

“Anhaa...mwenzako nimekaa hapa nakuwazia wewe tu unavyopitia mambo magumu vipi sasa itakuwaje?”

“Kuhusu nini tena?”

“Kuhusu wewe kuondoka, maana najua unatamani kuondoka na hauna hela”

“Mh...hilo usijali...wewe waza tu mambo mengine wala mimi nisikuumize sana kichwa sawa? We soma kwa bidii umalize uwe doctor...naamini utakuwa daktari mzuri sana” 

“Maulid....umekula?”

“Nimekula niko vizuri” Maulid aliamua kumjibu vile lakini kiukweli tangu mchana hakula chochote, kwani hakuna wa kumpatia

“Sawa, samahani nimeshindwa kuja niko mbali”

“Uko wapi?”

“Niko, huku kwa ba mdogo, forest, ila kesho asubuhi nitakuwa hapo nitakuletea chakula sawa?”

“Sawa”

“Nakupenda sana” binti alijibebisha, alikuwa hafurukuti kwa mwamba hata kidogo

“Asante. Nakupenda pia” alisema Maulid lakini hakutaka kumpotezea muda binti, aliamini sio type yake tena

Baada ya kukata simu mtoto wa kike roho ilizidi kumuuma, kiukweli Maulid misaada mingi maana hakuwa na pesa ya kulipa hospitali, hakuwa na sehemu ya kushukia, na hakuwa na kazi. Kwa hiyo ilimuwia Tricia vigumu kuweza kumsaidia lakini aliamini anaweza kwa njia yoyote
........JE ATAFANYAJE TRICIA????
KIPENGELE CHA 15
Tricia bila uoga alimpandia baba yake hewani na kuanza kuongea naye mambo mengi, lakini mwishoni binti alimpiga kizinga baba yake

“Baba...huku kwa baba mdogo ni mbali sana na hospitali”

“Kwa hiyo?”

“Ah nilikuwa nawaza kupanga karibu na mjini kwa ajili ya kujisomea na wenzangu....”

“Mh Tricia, kwanini hukubaki Dar?” aliuliza

“Hamna baba...nilishakuambia sababu”

“Ah, haya bwana kwa hiyo unahitaji kupanga ushapata chumba?”

“Hapana, sina hela daddy, nilikuwa naomba unisaidie, nipange...naomba unitumie hela”

“kama kiasi gani kinahitajika”

“Huku kidogo vyumba sio ghali sana, ila cha elfu themanini kitanifaa sana...kwa hiyo nilikuwa naomba kama milioni mbili baba yangu nipange”

“Ahaa...sawa...basi hamna shida kesho asubuhi nitakutumia” mzee kwake kutuma pesa kama hiyo ilikuwa ni pesa ndogo kabisa.

“Thanks daddy God bless you”

“Sawa....ufikirie pia biashara zako uniambie kama unaweza tufanye hata uweze kuendelea kupata pesa zako binafsi”

“Sawa baba nitafanya hivyo”

“Ok good night”

“You too daddy”

Binti alikata simu akafurahi sana, baba yake hakuwa ubahili wa Kipare, alitiririka tu pesa ilipohitajika lakini kichwani binti alikuwa na lengo la kumsaidia Maulid atoke pale hospitalini akapate na sehemu ya kukaa.

*
Kesho yake saa kumi na mbili asubuhi, Tricia alikuwa ameshajiandaa kuelekea mjini kwa ajili ya jukumu lake la kila siku, ndipo akamtumia ujumbe baba 
“GOOD MORNING DADDY...PLEASE REMEMBER THE PROMISE...I LOVE YOU” alisema mtoto wa kike kumkumbusha baba yake amtumie kiasi cha fedha halafu aliaga nyumbani kuelekea mjini.

Akiwa kwenye gari, alisikia ujumbe kwenye simu, alipoangalia hivi, alikuwa baba amemuwekea kiasi cha shilingi milioni mbili na laki tano kwenye akaunti yake, alifurahi sana.

Alipofika mjini alinunua dawa moja ya kuondoa makovu, katika pharmacy kubwa pale mjini halafu alienda nayo hospitalini akampatie Maulid. Alipofika bila hata kwenda kumuona daktari, binti alipita kwanza kwenye chumba ambacho Maulid alikuwepo, nia yake ni kumsalimia na kumueleza kwamba atamlipia pesa zote na atampa maisha pia ya kuanzia pale mjini, hii yote binti alikuwa anafanya kwa sababu ya mapenzi si kingine. Aliamini mapenzi ni kumfurahisha unayempenda.

Binti aliingia moja kwa moja hadi katika chumba kile, lakini hakumkuta mgonjwa wake akiangaliwa wagonjwa wengine wanamshangaa, akatoka haraka akijua labda yuko uani
“Ngoja nitakuja baadaye” alisema kwa furaha na kuelekea ofisini lakini njiani akakutana na nesi akamuuliza
“Kwa hiyo ukaamua umtoroshe”

Tricia akashangaa na kuuliza “Nimtoroshe????”

“Ndio”

“Nikaamua nimtoroshe nani?”

“Mh...si Maulid?” aliuliza

“Maulid? Kwani Maulid katoroka?” aliuliza binti kwa mshangao

“Kumbe hujui” alisema nesi na kuendelea na safari zake,

Kwa kifupi alipata simanzi mtoto wa kike baada ya kuambiwa vile, lakini alitaka akathibitishe kwa doctor mkuu, akamfuata ofisini

“Doctor shikamoo”

“Marahaba kwema?” aliuliza doctor huku akiuma mfuniko wa peni kama kawaida yake

“Kwema” alisema kwa wasiwasi ndipo doctor akatabasamu

“Hivi yule Maulid ni mtu wa wapi?” aliuliza

“Mh.....mi sijui...ila eti ametoroka??”

“Nani kakuambia?”

“Adela”

“Haha..nilijua tu....vijana wengi wa style ile lazima watoroke tu....”

“ameondoka saa ngapi?”

“Usiku kama nilivyopewa taarifa”

“Walinzi walikuwa wapi?”

“Yaani...mimi hata sielewi utaratibu huu uliletwa na nani....sawa tutafuatilia kama atapatikana...ila najua ni mtu wako na unajua alipo”

“Haki ya Mungu sijui alipo kweli doctor....” alisema binti kwa kuapia

“Haya bana” alisema doctor kwa kukata tamaa
JE MAULID KATOROKA KAENDA WAPI? ITAENDELEAAAA

FURAHA YANGU ILIPO
SEASON TWO 16 HADI 18

Na Mr AB ENTMENT

KIPENGELE CHA 16

TULIPOISHIA
“Walinzi walikuwa wapi?”

“Yaani...mimi hata sielewi utaratibu huu uliletwa na nani....sawa tutafuatilia kama atapatikana...ila najua ni mtu wako na unajua alipo”

“Haki ya Mungu sijui alipo kweli doctor....” alisema binti kwa kuapia

“Haya bana” alisema doctor kwa kukata tamaa

ENDELEA HAPA
Ilikuwa ni siku ya simanzi tena kwa mtoto wa kike, alikuwa hajui kwanini kila mara penzi lake na Maulid linapokolea basi ndio huchoropoka na kukimbia kabisa katika uso wake, aliumia sana.

Alitoka nje akakaa chini ya mti peke yake akawa anawaza mambo mengi sana kuhusiana na Maulid, hakujua mtaalamu kaamua kukimbilia wapi tena

“Hivi kwanini unakuwaga na tabia za kupotea bila taarifa?” binti aliuliza nafsi ambayo hata ilikuwa haimsikii “Si ungeniambia tu unaondoka nijue? Aah au kisa mi nakupenda?” alizidi kuongea mtoto wa kike roho ilikuwa ikimchoma sana, ya nini mtoto mdogo kujifia na presha kisa mapenzi.

Alijaribu kujizuia kwa namna yoyote lakini kiukweli ilikuwa ni hali ngumu sana kuzoea kuishi bila kumuona Maulid kwa mara nyingine alikuwa anatamani kuwa naye katika maisha yake yote, lakini amepotea kwa mara ya pili

“Mi nitakuona wapi?” alisema binti “Ina maana wewe hunipendi kama mimi ninavyokupenda ndo maana ni rahisi kwako wewe kutoroka na kwenda mbali kila saa khaa” alisema kwa sauti ambayo ilionyesha kusikitishwa na mapenzi wakati wote.

Kiukweli Tricia alikuwa amekufa ameoza na sababu alikuwa hajui ni ipi. Unaambiwa baada ya Maulid kuondoka tena, ilipelekea binti kuumwa siku nzima yaani yupo yupo legelege mpaka doctor alipomuonea huruma akamuambia aende nyumbani akapumzike.

Tricia alipanda gari na kwenda nyumbani, bado alipata mawazo ya kishetani, na hata kuamua kumtumia ujumbe Samawati akamuomba namba ya Maulid kwa sababu aliamini bado hajaifuta licha ya kumtelekeza hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili.

Samawati wala hakujibu ujumbe wa Tricia.

Jioni mida ya saa 12 Tricia alipita katika mtandao wa instagram alikuta chapisho lililochapishwa na ukurasa wa JamiiForums likiandikwa hivi “Mbeya: AKUTWA AMEJINYONGA MSITUNI, CHANZO UGUMU WA MAISHA”

Unaambiwa moyo wa Tricia ulipiga paah....kwa haraka haraka alihisi ni Maulid, alisoma maelezo ya haraka haraka “Mwili wa kijana anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 29 hadi 31 (jina halijafahamika bado) wakutwa katikati ya vichaka vya Kyela akiwa amejinyonga, huku akiacha ujumbe kwenye karatasi kwamba katika maisha yake hakuwahi kufurahia isipokuwa mara moja tu, siku alipofaulu kidato cha nne, aidha kijana huyo alihusisha umasikini kumpelekea yeye kujinyonga”

“JESUS” alisema mtoto wa kike huku akiweweseka kwenye gari, hajui afanyeje, alijikuta machozi yakimtoka anateseka hakuwahi kupenda tena, ndipo akampigia simu Samawati lakini Samawati alikuwa bize muda wote binti akagundua kwamba amemblock kabisa, ikabidi aazime simu ya abiria mmoja ndipo akampigia Samawati akapokea

“Dada shikamoo” alisema Tricia huku akitetemeka

“Marahaba...nani?” aliuliza Sama

“Mi Tricia please naomba uniambie kama unafahamu Maulid alipo maana ametoroka hospitalini”

“Mi sijui”

“Please naomba unitumie namba yake nimtafute”

“Haipatikanagi hii niliyo nayo”

“Uwiii” alisema Tricia huku akikata simu, alikuwa ameshapatwa na wazimu kabisa, alikuwa kama amechanganyikiwa mtoto huyu, hakika alikuwa na wenge lililopitiliza.

Alipofika nyumbani alishuka kwenye gari akakimbilia nyumbani haraka na kuingia chumbani akajifungia halafu akapiga magoti
“Yesu...roho yangu hii...msaidie Maulid huko alipo awe salama mi ninampenda eti...” alisali huku akilia kabisa hajui amepatwa na nini mwanamke yule

Alifanya jitihada zozote za kumpata lakini wapi binti alikuwa hampati Maulid, alichanganyikiwa

********
Siku zilisogea zikasogea, na kutembea kwa kasi, hadi wiki mbili zikawa zimeshakatika, Tricia akawa ameshaanza kusahau maswahibu ya mapenzi kabisa na hakutaka kurudiana na Frank, aliamua kuwa serious na maisha kabisa, alikomaa na kilichompeleka Mbeya kuliko mapenzi.

Tricia alimfuata kijana mmoja dalali, akamtamfutia chumba karibia na mjini ili aweze kufanya kazi kwa amani, alihitaji pia kujifunza kujitegemea... kwa bahati nzuri alipata chumba na maisha yalisonga mbele....ni kazi, kusoma na sala kwenda mbele alikuwa hana haraka na mapenzi tena, alijiona alivyokuwa anaweweseka usiku mzima bila hata kumpata aliyekuwa anampenda

Siku zilizidi kutembea mpaka mwezi ukakatika, Tricia akawa amesahau kabisa masuala ya mahusiano, yeye na Frank waligeuka maadui, ni salamu tu na kupitana, watu hawakuamini kwamba ingekuwa hivyo.

Siku moja Frank alimtumia message binti na kumuuliza “Ina maana kweli Tricia ndio imeshabaki kuwa story?”

Tricia akajibu “Ndio...mi siwezi kurudi kwako tena. Hapa moyoni mwangu nimegundua kuna mwanaume mmoja tu...asipotokea sitakuwa na mwingine....na akijitokeza ninambebea tu mimba”

“Duuh....mwanaume mwenyewe inawezekana amejiua kweli. Maana nilipomtorosha pale hospitali usiku alikuwa akidai kwamba hawezi kuishi na stress zote hzo”

“Acha ujinga wewe....hata kama amefariki siwezi nikawa na wewe...halafu kumbe wewe ndiye ulimtorosha mjinga wewe ili asiwe karibu na mimi”

“Hahah....ndo ukome” alisema Frank

“Pumbavu wewe....na siwezi kuwa na wewe sasa”

“Hata usipotaka kuwa karibu na mimi kwani kipi nisichokijua kwako? Uchafu wote wa kwako naujua” alisema Frank maneno ambayo nusu yamtoe roho binti, akawa mpole

“Sasa huo uchafu ndio hautouona tena...na naomba uniheshimu sihitaji maneno na wewe Frank”

“Kwendraa....mimi mwenyewe ningekutaka ningekuacha uhame?”

“Unanitaka ndo maana unanitafutaga kila siku....”

“Nakutafutaga nikupime tu kumbe huna akili Tricia”

Tricia kwa hasira aliiblock ile namba ya Frank halafu akajilaza kitandani, alikuwa na hasira kweli kweli....aliona jinsi gani mwanaume ana dharau pale anapokutumia halafu baadaye mnagombana, aliumia sana Tricia na kujikuta anakuwa mdogo kama piritoni.

Akiwa amejilaza kitandani mara akasikia ujumbe kwenye simu, akaivuta simu na kuufungua akakuta ni wa namba mpya, ilikuwa hivi “MAMBO MREMBO”

Tricia akajibu kwa mkato “P NANI??” yote haya yalichangiwa na stress alizopata kutoka kwa Frank

“P ndio nini? Si ujibu kisomi?”

“Oya...unasikia? kama umetumwa useme mimi sijasoma kuja kujibu message zako kama hutaki kujitambulisha basi kausha kimya mimi nina stress zangu”

“Hahaa...pole and I am sorry for all....mi Maulid”

Hii message ilisababisha binti akaketi kitandani bila kutarajia halafu akauliza “Maulid?????”

“Ndiyo....nimekukumbuka leo nikasema nikutafute”

“Mmmmh....bhana” binti alijikuta amerudi kwenye mudi ghafla, akajaribu kuipigia ile namba mara ya kwanza lakini haikupokelewa
JE HUYU NI MAU KWELI AU NI MTU ANAMCHORA?
EMBU TUONE KWENYE KIPENGELE CHA 17 HAPO KESHO

KIPENGELE CHA 17
Tricia alishtuka na kuhisi labda ni Frank anamjaribu kwa kutumia namba nyingine. Alimtumia ujumbe “Mbon hupokei simu kwanza wewe sio Maulid”

“Ngoja nakupigia subiri kidogo” alisema huyo mtu kwa SMS

“Mfyuuu” binti alisonya akijua kabisa sio Maulid aliyekuwa anamtafuta, wala hakuijibu ile message rather aliingia kwenye mtandao wa TikTok akawa anaangalia angalia video ili aburudike kidogo.

Ilikuwa kama masihara lakini baada ya dakika kumi yule mtu alimpigia Tricia alipokea
“Hallo” alisema Tricia

“Hallo mambow” ilitoka sauti upande wa pili kweli ilikuwa ni ya Maulid, ilifanya moyo wa binti udunde kwa kasi ya ajabu

“Poa” alijibu huku akitetemeka

“Uko wapi? Nimekumiss sana” alisema Maulid

“Maulid....Maulid.....Maulid nimekuita mara tatu”

“Hahaha...najua huamini”

“Siamini kivipi? Mi kwanza umeniudhi umenikera....sikutamani hata unitafute” alisema binti akijifanya eti alikuwa hatamani jamaa amtafute, wakati alihangaika muda mrefu sana kujaribu kumpata

“Samahani...najua labda nil....” kabla hajamalizia sentensi simu ilikatika, na kilichofanya ikakatika ni salio liliisha kwenye simu ya Maulid

Tricia na hasira zote, akapanda hewani “Wewe mbona umekata simu?”

“Dakika zimeisha”

“Enhee...kwanini ulitoroka...? unajua mimi watu wanasema ndo nilikutorosha? Unajua nimeteseka kiasi gani kuhangaika kukutafuta ulipo? Unajua nimefikiria mambo mangapi mpaka nikahisi wewe umekufa? Kweli Maulid mimi ni wa kunifanya nikose amani? Mimi ndiyo wa kunitesa kila wakati?” alisema binti kwa hasira tena akilia

“Nisamehe Tricia, labda nimekuwa tatizo kwenye maisha yako...lakini kiukweli ninashukuru sana kwa mambo ambayo umekuwa ukinifanyia....leo nimekuwa mzima wa afya ninapambana kutafuta riziki, ninakukumbuka sana...please nisamehe ulijua hali niliyokuwa nayo pale hospitalini, sikuwa na chaguo zaidi ya kukimbia tu”

“Daaah” alisema binti “Ulikimbilia wapi wakati ulikuwa wewe ni mgonjwa??”

“Niliondoka nikaenda kwa wanangu ambao tulikuwa tunafanya nao uvuvi kipindi cha nyuma, nikakaa pale kwa muda mrefu mpaka nikapona kabisa, sasa hivi mguu unauma kwa mbaali, lakini nafanya kazi vizuri”

“Uko wapi??”

“Niko Kyela”

“Kyela?? Mbona mbali?? Mi siamini kama wewe ni mzima eti...nataka nikuone tu kwa macho hivi” alisema mtoto wa kike

“Usihangaike bana wewe pambana tutaonana tu” alisema Maulid

Binti akaja juu “Hivi wewe haunipendi ee? Hivi unakuwaje kirahisi rahisi tu unaniambia nisihangaike?? Ungekuwa unaumia kama mimi au ungekuwa unanipenda basi ungetamani hata kuniona tu...lakini sawa bye” binti alisema kwa hasira

“Samahani...nakupenda sana basi sawa kama unataka tuonane njoo mi sijakukataza..natamani kukuona pia”

“Bhana mimi ushaniudhi unaonekana kabisa hata haunimiss”

“Nakumiss....njoo please mi naogopa kuja huko mjini si unajua niliondoka na deni la watu?” alisema Maulid

“Mi wikiendi nakuja utanielekeza...si unapatikana namba hii?”

“Ndio...nitakuambia”

“Ok sawa.....mi nimebaki naangalia picha zako tu”

“Bora wewe...mi hata picha sinaga...ukija uniletee picha maana natumia simu ndogo, safisha picha uniletee...sawa?”

“Sawa....lakini kwani namba yangu umepata wapi?” aliuliza Tricia

“Ah...siku ile ulipompigia yule nesi pale hospitalini ukamuambia anipe simu ndo niliiandika kwenye karatasi changu”

“Mh wewe mtundu”

“Hahaa...hapana ni kwa sababu wewe ni mwanamke wa kipekee kwenye maisha yangu”

“Sawa bhana”
*
Ilikuwa ni safari ya matumani, hatimaye mawasiliano yalirudi kati ya wawili waliokuwa wakipendana sana.

Tricia alipanga safari yake vizuri, hadi ilipofika siku ya jumamosi, aliamua kujiandaa vizuri, alibeba zawadi kadhaa, akapanda gari pale nane nane, na kuingia Kyela kwa ajili ya kwenda kumtafuta Maulid

Ilikuwa ni safari ndefu, lakini ilikuwa ni safari yenye matumaini kidogo kwenye maisha yake, aliamini akishahakikisha kwamba Maulid yupo hai na ni mzima wa afya basi angeridhika kabisa na hata kujihisi vizuri zaidi. Alimpenda kweli.

Safari iligota Kyela, giza lilikuwa linaingia ingia binti alichoka nyang’anyang’a, baridi ni kali maeneo yale.

“Uwii mbona ni mbali hivi?” aliuliza Tricia

“Ni mbali sana...lakini karibu sana”

“Mh...nimechoka. Nilijua nitakuja na kurudi”

“Pole utaondoka kesho”

“Nitalala wapi?”

“Ninapolala tutalala wote au vipi?”

Tricia alimtazama Maulid halafu akacheka, alionekana ile sentensi ya kulala wote ilimfurahisha kidogo, maana ni muda alikuwa amemmiss sana.
“Makovu yamepungua usoni, lakini kila siku mwili wako unazidi kupungua Maulid”

“Maumivu makali ya maisha..ila nitarudi kwenye mstari soon”

“Unafanya kazi ya uvuvi tu?” alisema binti huku akitembea tembea kando ya barabara upepo ni mkali

“Ndio”

“Unapata hela sasa?”

“Ndio, najikimu” alisema Maulid halafu akamvuta kwa nguvu binti na kumkumbatia. Tricia alimdandia wakajikuta wote wanahema kwa nguvu hamna kitu kitamu kama hicho, maana kila mmoja alimmiss mwenzake.

“Twende ukale” alisema Maulid na kumuachia mtoto wa kike
Walienda mpaka kwenye mgahawa mmoja wakaagiza wali samaki halafu wakala na kuondoka mpaka geto.

Lilikuwa sio geto la Maulid, alikuwa akiishi na wenzake, lakini kwa kuwa siku ile walijua shemeji anakuja waliondoka na kwenda kulala sehemu nyingine mpaka atakapoondoka.

Siku ile Maulid alilala na binti usiku kucha, walipeana kila kiitwacho kitu....MI SITAKI KUTAJA SIRI ZA WATU...TUKUTANE KIPENGELE CHA 18

KIPENGELE CHA 18
Aubuhi ilipofika binti akamuambia “Unajua sina kinga?” 

Maulid akauliza “Kwani upo kwenye siku za hatari?”

“Ndio....ila mh nitatumia dawa” alisema binti

“Sawa...”

Siku ile Maulid alimchukua binti mpaka Matemba Beach wakaenda kubarizi kidogo....kulikuwa sehemu safi ya kupata upepo.

Walifurahia sana siku ile kuwa pamoja, ndipo baada ya muda wakaketi kwenye mtumbwi na binti akamlalia kifuani halafu akafumba macho

“Hivi Tricia kwanini unapenda kulala kifuani mwangu kila mara?”

“Baby....mimi nikilala hapa hivi nasahaugi shida zote...nilishawahi kukuambia kabla, kwamba furaha yangu ipo hapa kwako...ndio maana hata tukitengana muda mrefu, nikishakuona basi siwezi kuzizuia hisia zangu”

“mh...nikuambie kitu kimoja..mimi ninakupenda sana” alisema Maulid

“Ninakupenda pia” alisema mtoto wa kike

*
Baadaye binti aliondoka akarudi mjini Mbeya, nyuma alimuacha Maulid akiwa na furaha tele, alijua ameshafika pale alipokuwa anapataka, mapenzi yalitaradadi.

Lakini Tricia alipofika mjini alinunua dawa aina ya P2 dawa ambayo ikimezwa na mwanamke ambaye amepata mimba ndani ya masaa sabini na mbili, mimba huwa haishiki.

Alipomaliza alienda mpaka nyumbani, akafungua mlango na kuketi kitandani halafu akachota maji kwenye ndoo ili aweze kumeza dawa ile.

Alitazama dawa kwa muda wa sekunde thelathini, ndipo akazipiga chini kwa hasira “Aah...” kuna roho ilimuambia asimeze dawa zile. Alikunywa maji tu akaoga na kupumzika zake huku akimtaarifu Maulid kwamba ameshafika nyumbani.

*
BAADA YA MWEZI MMOJA
Mara kadhaa Maulid alikuwa anamtembelea Tricia mjini na hata kukaa kwa siku mbili halafu kuondoka, ilikuwa ni fursa nzuri kwa Maulid kumfaidi mtoto ambaye alishamkosakosa mara nyingi sana, penzi halikuisha.

Kwa bahati mbaya au njema kwa upande mwingine, binti aligundua ana mimba ya Maulid, japo alishtuka kidogo, lakini alijua kabisa kwamba anatakiwa kumzalia maana ni mwanaume ambaye amempenda muda mrefu na hata wakipotezana aliamini atakuwa amemuachia alama nzuri katika maisha yake

“Sasa...kama una mimba itakuwaje?” aliuliza Maulid wakati binti alipompa taarifa kwenye simu

“Itakuwaje kivipi??”

“Yaani namaanisha utatoa au utazaa?”

“Hunipendi?? Kwa hiyo wewe unataka nitoe?”

“Sio hivyo, natamani kuitwa baba...lakini siwezi nikaitwa baba bila wewe kukubali, inawezekana umeishika kwa bahati mbaya tu na ukawa haupo tayari”

“Hapana nipo tayari...au kama wewe hautaki nitafanya kutoa”

“Nataka, ila nawaza kuhusu mzee wako”

“Mh yule achana naye,....nitamueleza baadaye kwamba ana mjukuu”

“Akijua ni mimi si itakuwa ni vita?”

“Ah usijali sisi si tupo mbali huku jamani? Atakuuaje? Nitampa taarifa tu”

“Sawa....ila usimuambie kwanza”

“Okay”

Binti alikata simu na kuwaza mambo mengi sana...alijua baba yake hapendi utani kabisa kwenye maisha, alitambua akimuambia kwamba ana mimba basi itakuwa ni kasheshe.

Mawazo yalimjia, aidha atoe ili awe na baba au aishi nayo achukiwe na baba, lakini alijiuliza, je kwa tatizo la ajira hata akimaliza kusoma udaktari anaweza kujikimu bila kumtegemea baba?

Ilimpa wakati mgumu kuhusu hatua ya kuchukua juu ya ule ujauzito.....JE BINTI ATACHUKUA MAAMUZI GANI KUHUSIANA NA DUDUKE??
USIKOSE KIPENGELE CHA 19

Post a Comment

Previous Post Next Post