SEASON TWO 04 HADI 06
Na Mr. AB
KIPENGELE CHA 04
TULIPOISHIA
“Daah...kwa hiyo hujui lolote kuhusu Johnson na Musa?” aliuliza
“Sifahamu kwani kuna nini man?” aliuliza kwa mshangao mkubwa
“Mzee,....sisi wenyewe tulishangaa kukuona, tulijua labda ulikuwa nao...mbona walipata ajali Makambako wakafa aisee...muda mrefu sana?” aliuliza kijana huyo
“Wamekufa????” aliuliza kwa mshangao Maulid
ENDELEA
“Duuh” yule bodaboda alisema kwa hasira na kugeuka “Kwa hiyo mwanangu mi nakuambia masihara?” alisema
“Daaah......embu kwanza” alisema Maulid akimfuata, ashaanza kuogopa, akamshika mkono na kumvutia pembeni “walikufa lini? Kwa sababu gani masta?” aliuliza huku machozi yakimlenga lenga
“Mzee....mliondoka wote...ila baadaye wakiwa wanarudi walipata ajali wakafa,....tena sisi tunajua na wewe ulikufa ndo maana tunakushangaa”
Akiwa anaongea vile Maulid alishtuka, watu walikuwa wamemzunguka wote wanamuangalia, wanataka kujua ilikuwaje mpaka wakafariki halafu yeye bado akawa hai tena mzima wa afya kabisa
“Mi sielewi jamani...mi sielewi” alisema Maulid huku akikuna kichwa na kutokwa na machozi akasema “Ina maana Musa na Johnson wamekufa?” aliuliza tena lakini watu wakawa wanamshangaa.
Yalikuwa ni maumivu yaliyokisiri kwa kijana Maulid, suala la kufiwa na marafiki wa karibu ni suala gumu sana, ni suala ambalo halivumiliki. Johnson na Musa walikuwa marafiki wa Maulid kwa kipindi cha miaka mingi, wamefanya biashara ya mkaa kwa muda mrefu, wamepambana pamoja.
Maulid alijikuta anawaza mambo mengi yaliyompelekea kusikia kichwa kinauma, huku maumivu makali ya moyo yakimuandama.
Alishindwa kuelewa afanye nini, alitembea tembea akarudi na kusimama katikati ya mji halafu akajisemea kwa sauti ndogo “Daaah....ilikuwaje mpaka wakapata ajali? Au walikuwa wamelewa? Daaah wanangu ina maana.....hapana hapanaa” alilia kwa uchungu hakujua afanye kitu gani.
Alitembea anataka kwenda stendi ndipo akapita kwa yule mama lishe akamuita “Mama Rama”
“Abee”
“Niambie hivi Johnson na Musa wako wapi?”
“Johnson na Musa walifariki muda wa miaka miwili iliyopita, ina maana hauna taarifa?” aliuliza mama Rama hapo ndipo kweli Maulid kaamini ni kweli....hakumjibu chochote aliondoka moja kwa moja kuelekea stendi ili aweze kupata gari ya kuelekea Mbeya.
Alipopata gari alikuwa na mawazo mengi, stress za hapa na pale, akiwaza jinsi alivyokuwa amezoeana na marafiki zake.
Maulid alifikia mahali akawaza jambo la msingi kidogo, alikumbuka siku ya mwisho alipokuwa anasubiriwa na kina Musa na Johnson, alijiandaa vizuri lakini wakati akiwa anapanga nguo zake, alikuja Tricia na ilikuwa mara ya kwanza kulala na Tricia.
Hii ilipelekea Maulid kuahirisha safari yake na kubaki jijini Dar, huku kina Johnson na Musa wakimlaumu.
Baada ya hapo Maulid hakuwahi kuwasiliana nao tena.
“Ina maana siku ile ndo walienda kufa?” alijiuliza “Kwa hiyo na mimi ningekuwepo basi ningeshakuwa nimekufa” aliendelea kuwaza mambo kibao huku akikumbuka matukio mengi waliyowahi kufanya kwa pamoja “Ila mi fala....kwanini sikwenda nao huenda ningeendesha gari mimi na yote yasingetokea” alijisemea moyoni “Labda Tricia aliniokoa na kifo ....” aliwaza mambo mengi na kwa mbali alikuwa anamuwazia Tricia mpaka pale usingizi ulipokuwa unampitia taratiiibu mpaka akapotelea usingizini kabisa safari ikizidi kuendelea.
Wakati yeye, Maulid akiwa katika usingizini, kumbe Tricia yeye alikuwa na Frank Bukuku walikuwa katika kitanda cha Frank. Tricia alikuwa ameketi huku huku Frank akiwa amemlazia kichwa mapajani. Na Tricia alikuwa anamkamua chunusi/vipele vilivyokuwa usoni mwake vichache
“Ssssh...kinauma” alisema Frank
“Tulia bwana...wewe ni mwanaume unaumia nini?”
“Kanauma sana....na wewe unafanya kwa nguvu sana...bonyeza taratibu...hujui hata kumbembeleza mdomoni” alisema Frank.
Tricia aliachana na zoezi la kumkamua vipele akaanza kumtania huku akishika vindevu vichache ambavyo Frank alikuwa navyo kidevuni
“Achana na hizo ndevu”
“Hahaa...eti ndevu...vindevu vyenyewe ni vidogo sana hivi..vinaanzia huku vinashuka mashavuni mpaka zinakutana na hizi zingine” alisema binti huku akipitisha kidole kutoka sikioni akakishusha shavuni mpaka kidevuni
“Kwa hiyo sina ndevu mimi?” Frank aliuliza huku akimtazama
“Hakika hizi sio ndevu za mwanaume...mfano Maulid alikuwa na ndevu nyi.....” kabla hajamalizia sentensi alijishtukia na kuacha kuongea, alikuwa amemtaja mpenzi wake wa kwanza kabisa, kijana Maulid Khamis Zabuni
“Mh huyo Maulid umemmiss sana...hivi kwanza unavyomtaja kila mara, si mkikutana unampa wewe? Kwanza si nitaachwa mie?” alisema Frank huku akiinuka kutoka mapajani mwa binti
“Hapana siwezi kumpa...siwezi rudiana naye...aliniacha vibaya halafu pia yule sio type yangu”
Frank alimtazama usoni Tricia, na Tricia alimshika shavuni na kumuambia “Usikasirike mi nakupenda kweli ndo maana nimeamua kuja na wewe huku Mbeya, ili unifaidi” alisema
“Kweli?” Frank aliuliza
“Ndio baby” binti aliongea na kumsogelea akambusu shavuni.
*
Jioni muda wa saa kumi na mbili na nusu, Maulid alikuwa ameshatimba jijini Mbeya, alikuwa na njaa kweli kweli, alikuwa anakatiza katika mtaa mmoja, ambapo alikuwa anataka akae mahali amsubiri Samawati ambaye alikuwa amemuambia kwamba bado yuko hospitalini anamuangalia mtoto wake.
Muda huo Samawati alikuwa hospitalini, na alikuwa ameketi kando ya kitanda cha mgonjwa ambaye ni mtoto Maulid, na muda huo pia ndiyo Tricia alikuwa ameingia hospitalini pale maana alikuwa amepewa shift ya usiku, lakini Frank yeye alikuwa na ya mchana hivyo hakuwepo pale.
Mama Maulid, au kwa jina lingine Samawati alitoka hospitalini haraka haraka na kwenda nje ya geti akachukua pikipiki ili awahishwe kwenda kukutana na Maulid. Target yake kubwa ilikuwa ni kwenda kulala na Maulid, ili ampatie mimba akiamini atapata mtoto wa kike.
Baada ya dakika kumi tu, alikuwa ameshakutana na Maulid, walikuwa wanatembea kuelekea katika nyumba ya wageni, ndipo binti akafungua pochi yake ili kuangalia pesa ya kwenda kulipia.
Alipokuwa anafungua pochi ghafla aligundua kuwa simu yake haipo “Hee...simu yangu” alisema kwa mshtuko kidogo
“Vipi tena?” Maulid aliuliza
“Simu nimeacha wapi tena?” alijiuliza kwa mshangao halafu akaondoka
“Haipo?” aliuliza Maulid
“Ndio.....embu please nipigie?” alisema akianza kuogopa binti
Maulid haraka haraka akaitoa simu yake mfukoni kisha akampigia Samawati kwenye namba yake, ikaita
“Inaita” alisema Maulid
“Inaita? Embu” alisema Sama na kuipokea simu halafu akasikilizia kama itapokelewa.
Kweli ilipokelewa na ilikuwa sauti ya mwanamke
“Hallo...” alisema Samawati
“Hallo vipi...” aliuliza upande wa pili
“Safi samahani, hiyo ni simu yangu ninaomba” alisema
“Sawa, umeisahau hapa hospitalini...njoo uchukue”
“Sawa dada yangu....asante” alisema kwa uchangamfu halafu akakata
“Vipi nani?”
“Kumbe niliisahau hospitalini” alisema “Twende”
Safari ilianza wakaondoka moja kwa moja mpaka hospitalini
Kumbe muda wote aliyekuwa amepokea simu ya Samawati alikuwa ni Tricia, na Samawati alipofika moja waliingia ndani ya hospitali, na kumpigia tena akapokea Tricia
“Hallo....tuko hapa nje, naomba uniletee hiyo simu tafadhali”
Tricia akasema “Sawa...nakuja sasa hivi”
ITAENDELEA
KIPENGELE CHA 05
Wakati wakiwa wanamsubiri, kwa bahati mbaya au nzuri, Maulid alipokea simu kutoka kwa kijana mmoja ambaye walikuwa wakivua naye samaki kitendo kilichomfanya asogee pembeni kidogo na kukaa sehemu ambayo kulikuwa hakuna kelele.
Akiwa pale aliongea kwa dakika kama tatu, ndio akajitokeza na kumuangalia Samawati alikuwa anashangaa shangaa.
Maulid alimfuata na kumuuliza “Vipi?”
Sama akajibu “Ameshanipatia”
“Ni nani huyo?” aliuliza
“Yule binti kule” alisema huku akinyoosha mkono kuonyesha binti alipoenda, kwa mbaali Maulid alimuona binti akiwa anatembea, lakini kwa sababu mwanga wa taa ni hafifu kuliko wa mchana, hakufanikiwa kumuona vizuri, ila kutokana na mwendo ambao Maulid aliuona miaka kadhaa wa binti Tricia, alijikuta anamshangaa licha ya kumuona upande wa nyuma tu
“Ni nani?”
“Ni nesi sijui” alisema Samawati “Ana roho nzuri, nimempa hela ya shukrani akakataa kata kata” alisema binti
“Okay....twenzetu”
Samawati pamoja na Maulid walienda mpaka katika lodge moja wakalipia kisha wakala vizuri na kwenda kujipumzisha kwa usiku mzima.
Asubuhi sana, Maulid na Samawati waliamka na kwenda kupanda gari wakaenda katika majukumu yao ya kila siku.
Mchana siku hiyo ya Jumatatu, Isaac Mwaipopo ambaye alikuwa ni mdogo wake Dr Joseph Mwaipopo, alikuwa amekaa nyumbani kwake amepumzika huku akiwa anakula wali na parachichi, akampokea simu kutoka kwa kaka yake
“Baba Tricia” alisema Isaac baada ya kupokea simu
“Naam...unaendeleaje ndugu yangu?” aliuliza baba Tee
“Niko salama kabisa, huko Dar es Salaam vipi?”
“Huku tuko salama kabisa....samahani uko bize au upo free?” baba Tricia aliuliza
“Niko nyumbani nakula zangu chakula cha mchana, karibu bwana” alisema
“Asante sana....aah mmh hivi binti yako ameshawahi kufika hapo nyumbani?” aliuliza mzee
“Tricia?” Isaac aliuliza
“ndio”
Isaac alifikiria kwa muda wa sekunde kadhaa, akasema.... “Kwani vipi? Mmeshaongea naye?” aliuliza
“Hapana, nampigia simu hapokei, anadai yuko bize, ndo maana nikasema nikupigie ili angalau kujua kipi kinamsibu”
“Ahaha....sawa, ni kweli yuko bize embu samahani kidogo ninakupigia sasa hivi kuna mtu ananipigia” alisema Isaac
“Sawa”
Isaac alikata simu kisha akampandia Tricia hewani haraka halafu akamuuliza “We Tricia wewe”
“Shikamoo baba mdogo”
“Marahaba...uko wapi?”
“Niko tu, nimekaa”
“Hospitalini au wapi?”
“Niko nyumbani kwa rafiki yangu”
“Sasa sikiliza, nimetoka kuongea na baba yako sasa, hivi ananiuliza uko wapi...nashindwa nimjibu haupo kwangu au la....nimemkatia nikasema nikuulize kwanza ili nisikusababishie ugomvi”
“Aaaah....ananiuliza kila mara...lakini anyway mwambie niko kwako”
“Hivi Tricia ina maana hautaki kuja kumuona mama yako? Hautaki hata kuwaona wadogo zako, kwanini? Yaani tangu tukutane pale mjini hujataka hata kuja tena”
“Nitakuja ba mdogo, lakini nimekuwa bize sana....leo nilikuwa free tangu asubuhi, lakini nilijua labda upo kazini...”
“Hata nikiwa kazini, ma mdogo wako yupo nyumbani muda wote” alisema Isaac
“Sawa, kesho nitakuja, ila niliogopa uliponiambia ni mbali siku ile”
“Sio mbali sana, gari shilingi 500 tu nauli jamani?”
“Sawa nitakujuza kesho”
“Okay basi, ngoja niongee na baba yako hapa”
“Sawa”
Isaac, alikuwa sio mtu wa shari, alikuwa ameamua kumfichia siri binti kwamba hajafika kwake maana aliamini akimuambia kaka yake, huenda ikaleta tatizo kubwa kwa binti.
Isaac alimpigia baba Tricia
“Enhee ushamaliza?” aliuliza Dr Mwaipopo
“Ndio...niambie sasa”
“Aaah...nimempigia Tricia sasa hivi nikakuta anatumika, anyway...ulisema yuko kwako hapo?”
Isaac kabla hajajibu alitabasamu kwanza maana mzee aliposema amempigia Tricia akawa anaongea na simu nyingine, aligundua kuwa binti alikuwa anaongea naye.
“Ah binti ameenda huko hospitalini...ila yuko hapa kwangu kaka”
“Sawa hamna tatizo, basi akirudi mwambie anitafute tafadhali”
“Sawa kaka”
Mzee Mwaipopo alikata simu, Isaac akaendelea na maisha yake mengine.
Wakati Tricia akiwa amekaa pale ndani, alikumbuka kitu, kwamba wakati alipoikuta ile simu ya Samawati katika kitanda cha mgonjwa aliyekuwa karibu na Maulid mtoto wa Samawati, aliibeba akaondoka mpaka kwa doctor, akiwa kwa daktari anataka kumueleza ndipo ile simu ilipoita. Na alipoitazama alikuta ni namba ambayo ilikuwa imeandikwa Maulid.
Hakushtuka sana maana, ni kawaida kwa watu wengi kutumia jina moja tu...lakini kitendo tu cha kukumbuka jina la Maulid bado kilimrudisha kule kule ambapo alikuwa hapataki, alijikuta anamkumbuka mwamba, Maulid Zabuni na kujikuta anafikiria mambo mengi
“Hivi aliishiaga wapi?.....mh ila baba yangu....lakini inawezekana aliniepusha na vitu vingi.....aaaah hivi namkumbuka kumbuka wa nini Maulid” alisema binti kwa hasira halafu akasimama na kupakua chakula kwenye sufuria iliyokuwa jikoni
ITAENDELEEAA
WANGAPI WANATAMANI MAULID NA TRICIA WAKUTANE? USIKOSE
KIPENGELE CHA 06
Baada ya Tricia kula chakula aliamua kumpigia simu baba yake, akawa anaongea naye
“Daddy mnaendeleaje?”
“Mwanangu tuko salama lakini kiukweli nimekumiss sana, nilikuzoea mtoto wangu”
“Mimi mwenyewe nimekumiss baba...lakini najifunza kidogo kuishi mbali na nyie wazazi wangu maana najua ipo siku nitajitegemea mwenyewe...na nitakuwa mbali na hapo nyumbani”
“Ni kweli Tricia, lakini naamini unaendelea vizuri hapo kwa Ba Mdogo wako”
“Niko vizuri”
“Hamna tatizo? Maana kila nikikutafuta unasema uko bize...nilijua una shida ya pesa nikutumie kidogo ya kukusaidia”
“Nitakuambia baba”
“Sawa kila la kheri”
“Sawa”
BAADA YA SIKU TANO
Samawati alikuwa amenogewa na raha aliyompa Maulid siku walipokutana kwa ajili ya kumtafuta mtoto. Siku hiyo ilikuwa ni siku nyingine ambayo Samawati alitakiwa kwenda hospitalini kumuona tena mtoto wake ambaye alikuwa amelazwa.
Samawati aliondoka na Maulid kutoka ziwani na kuelekea Mbeya. Alipofika Mbeya ilikuwa ni jioni jioni, siku hiyo Tricial kama kawaida alikuwa anaingia tena usiku, na Frank alimuacha nyumbani.
Samawati alipofika mjini alilipia room katika hoteli halafu akamuacha Maulid na kuelekea hospitalini kumuona mtoto wake.
Tricia naye alikuwa ameketi kando ya kitanda cha mtoto Maulid akawa anamuuliza uliza maswali
“Mama yako ni yule ambaye alisahau simu hapa?”
“Ndio” alisema
“Mbona hajaja tena tangu siku ile?” aliuliza binti
“Hayupo yuko kazini kwake”
“Anafanya kazi wapi?” alimuuliza
“Sokoni huko...anauza samaki”
“Anauza samaki? Soko gani?’
“Mi sijui...sikai naye”
“Anhaa...unakaa na nani?”
“Nakaa na baba yangu na mama mwingine”
“Ok sawa mtoto mzuri”
Tricia alionekana kumpenda yule mtoto Maulid, aliongea naye muda mrefu halafu akaondoka zake, alipofika mlangoni alikutana na Samawati ndio anaingia pale ndani, akampita maana hakumjua kwa haraka haraka
Samawati akamuita “Nesi” alisema ndipo binti akageuka na kumtazama akagundua ndiyo yule aliyempatia simu siku ile
“Ah...mama Maulid si ndio?” aliuliza Tricia
“Ndio...kumbe unanikumbuka?”
“Ndio...nilikuwa napiga story na mtoto wako sasa hivi...ananiambia unauza samaki..mbona hujaniletea?” aliuliza binti huku akimtazama mkononi kama amebeba chochote kitu
“Hahaa..jamani sikujua kama unataka samaki...labda ungesema mapema”
“Haha...sina hata namba yako” alisema Tricia
“Okay...nitakupatia namba yangu kuna rafiki yangu ataleta kesho kwa hiyo nitamuambia akuchukulie sawa doctor?” aliuliza
“Hamna shida nitashukuru” Tricia alitoa simu kwenye lock halafu akamuuliza “Niandike namba 07”
“Ah...sifuri sita....tano saba....hamsini na mbili....thelathini na moja....tisini”
“Haya asante...nakutumia message now...mi naitwa Tricia” binti alisema
“Ok”
Tricia aliondoka na kumuacha Samawati akiwa anaenda kumuona mtoto wake kule ndani.
*
Kesho yake asubuhi, Tricia alitoka hospitali, akiwa ameshika pochi yake, pamoja na simu mkononi akiwa anaongea huku ameweka sauti kubwa (loud speaker)
“Ndio nimetoka tukutane basi tunywe chai huku huku” alisema binti akiwa anaongea na Frank muda huo
“Okay sehemu gani?”
“Kwenye ile hoteli yetu”
“Sawa...unapapenda!!!” alisema Frank
“Haha...ufanye haraka basi”
“Ok”
Frank alikuwa ameshajiandaa ndiyo anataka kwenda hospitalini maana alitakiwa aende asubuhi, lakini vile vile binti Tricia alikuwa anataka wapate kwanza supu asubuhi ile ndio aende nyumbani.
Maulid na Samawati waliingia katika hoteli moja, ya hadhi ya kawaida na kuagiza supu na chapatti...wakawa wanakunywa taratibu huku wakipiga story mbili tatu.
“Maulid nishajikuta kama nakupenda hivi”
“Unanipenda?”
“Ndio...napata penzi tamu kwako..ndio maana nimeamua turudie tena na tena...nitashukuru nikishika mimba” alisema Samawati na kunyanyua mkono anataka kumlisha Maulid
Wakati anamlisha Tricia na Frank waliingia pale ndani ya hoteli, binti akashuhudia live Samawati akamepelekea nyama na kijiko mdomoni mtaalam Maulid.
Alishtuka akamtazama, anahisi anamfananisha lakini ilikuwa hii ni kweli...binti aliduwaa na kujikuta ameganda kama kapigwa na shoti akawa anamshangaa Maulid.
Lakini Maulid alikuwa hajamuona binti maana macho aliyaelekeza kwa Samawati kabisa.....ITAENDELEA

N hatarii
ReplyDelete